Siku
moja baada serikali kutangaza uamuzi wa kulifungia maisha gazeti la
Mawio, Mhariri Mkuu wa gazeti hilo ambaye pia ni Mkurugenzi wa kampuni
ya Victoria Media inayolimiliki gazeti hilo, Simon Mkina ameeleza jinsi
walivyopokea taarifa hizo.
Mkina
amesema kuwa ingawa wamekuwa wakisikia habari za kufutwa kwa gazeti lao
kweye vyombo vya habari ikiwemo mitandao ya kijamii, bado hawajapata
taarifa rasmi kutoka serikalini kuhusu uamuzi huo ili wajue hatua
watakazoweza kuchukua.
“Sisi
ndio waathirika wa wakubwa wa taarifa hii. Kinachotushangaza ni kuwa
hadi sasa hatujapata barua yoyote ya serikali kuhusu jambo hili. Na sisi
tumemsikia Waziri Nape akitangaza kutufuta na kwakweli tumeshtushwa
sana,” alisema Mkina.
Aliongeza kuwa uongozi wa kampuni hiyo umepanga kukaa na kufikiria hatua sahihi za kuchukua kutokana na uamuzi huo.
Kadhalika,
Mkina amesema kuwa serikali inapaswa kuwapa taarifa ya maandishi kuhusu
sababu zilizopelekea kufutwa kwa gazeti lao na habari iliyosababisha
wafutwe.
Amesema
wanashindwa kufahamu ni habari gani ilisababisha wafutwe kwa kuwa
walikuwa wakipokea barua ya kujieleza karibia kila baada ya wiki mbili
kuhusu habari walizokuwa wanaziandika.
Alisema
kuna tofauti ya sababu zinazopelekea kufutwa na sababu zinazopelekea
kufungiwa hivyo wanataka kujua ni habari gani zilizopelekea wafutwa.
Waziri
wa Habari, Utamaduni, Michezo na Sanaa, Nape Nnauye alisema kuwa gazeti
hilo lilifutwa kutokana na kuandika habari za uchochezi na zenye utata
na kwamba wamiliki wa gazeti hilo wamekuwa wakionywa na serikali tangu
mwaka 2013 lakini hata majibu yao yalikuwa ya kiburi na dharau.
Mawio limefungiwa maisha kuanzia Januari 15 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment
paulmkale