SIMBA walianza kumsainisha Marcel Kaheza wa Majimaji, akafuatia Adam
Salamba wa Lipuli. Mashabiki wakaguna…aaah jamaniieee watacheza wapi
wote hao mastraika?
Huku na huku mara wakamshusha tena Mohammed Rashid wa Prisons, Yanga
wakaibuka wakaaanza kulalamika kwamba Simba wanatibua tu michongo yao
makusudi kwa vile wana mkwanja.
Wadau walikuwa wakigunia usajili wa mastraika hao watatu kwa vile wote
wana sifa zinazokaribiana na waliongoza kwenye timu zao msimu uliopita.
Salamba alikuwa na mabao sita pale Lipuli, Rashid alikuwa na 10 huko
Prisons na Kaheza 14 pale Majimaji.
Kumbe bwana hicho kilichofanyika siyo bahati mbaya ni mipango matata
sana ya mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji ‘MO’ kuhusiana na usajili
mpya wa kikosi hicho msimu ujao.
MO amewaambia viongozi wa Simba kwamba usajili wa msimu ujao anataka uwe
wa tofauti sana na ndiyo maana utafanyika na watu wachache sana akiwemo
yeye na Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘try again’ chini ya
muongozo wa ripoti ya makocha.
Kiongozi huyo anayefahamika Afrika nzima kwa utajiri na mbinu za
ujasiriamali amewaambia vigogo wa Simba kwamba anataka kila nafasi
uwanjani iwe na wachezaji wawili imara sana yaani aliyeko kwenye benchi
awe mkali kuliko aliyeanza ili iwe bandika bandua.
Championi Jumatano, limebaini kwamba huku akiendelea kusuka kikosi hicho
tayari mazungumzo baina yake na makocha kadhaa kutoka Ulaya Kaskazini
na Ubelgiji anaotaka waje kuinoa Simba yamefikia pazuri lakini ni siri
kubwa hata viongozi wengine hawajui ni nini kinaendelea.
“Kila nafasi anataka iwe na wachezaji imara sana yaani kwenye benchi
kuwe na straika mkali kuliko Okwi na Bocco. Na anataka hilo lifanyike
kwenye nafasi zote, kuwepo na vikosi viwili imara sana ambavyo
havitazuilika kwenye ligi za ndani na michuano ya kimataifa.
“Lakini hao wachezaji imekuwa ni siri sana anafanya yeye na Salim,
hakuna yale mambo ya kamati kama zamani,”alidokeza kiongozi mmoja wa
Simba ambaye aliongeza kwamba hata Obrey Chirwa wa Yanga alikuwa kwenye
mipango yao lakini wamesikia amepata dili Misri katika klabu kongwe ya
Ismailia,” kilisema chanzo hicho.
Habari za ndani zinasema kwamba MO ambaye ni Simba wa kulia machozi
hatumii tena kamati maalum ya usajili kama ilivyokuwa siku za nyuma ndio
maana mambo mengi yanakwenda kwa siri sana na habari zinasema amekuwa
akisisitiza hivyo pia ili kuepuka ‘cha juu’.
Habari zinasema kwamba viongozi wengi wa Simba ambayo imeshampiga chini
straika kipenzi cha msemaji wa Simba, Haji Manara, aitwae King Laudit
Mavugo wameafiki anachofanya MO kwa sasa kwenye usajili kwani kitajenga
timu imara ambayo itakuwa na ushindani mkubwa na itawasaidia kuonyesha
mabadiliko ambayo yameanza kuonekana kwenye uendeshaji.
Habari zinasema kwamba MO amepania kusajili mchezaji wa gharama yoyote
ndani ya Afrika na hata kwenye mkutano mkuu wa wanachama alithibitisha
hilo na kupigiwa makofi yenye kilo nyingi.
Simba ambayo itashiriki michuano ya Kagame inayoanza Juni 29, Jijini Dar
es Salaam, inajiandaa pia na Ligi ya Mabingwa Afrika inayoanza Desemba
mwaka huu badala ya Februari kama ilivyozoeleka.
Baadhi ya timu ngumu za Afrika ambazo mpaka sasa zimefuzu Ligi ya
Mabingwa Afrika msimu ujao ni pamoja na Esperance na Club African za
Tunisia, Al Ahly na Ismailia zote za Misri.
No comments:
Post a Comment
paulmkale