Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dkt. Mwinyihaji Makame
akifungua pazia kuashiria ufunguzi wa jengo jipya la wagonjwa wa nje
katika Hospitali ya Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja kwa niaba ya Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ikiwa ni miongoni mwa
shamrashara za sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar. Alievaa miwani ni Naibu
Waziri wa Afya Mhe. Mahmoud Thabit Kombo na Daktari dhamana wa
Hospitali ya Kivunge Tamim Hamad. Picha na Makame Mshenga-Maelezo
Zanzibar.
Muonekano wa sehemu ya mbele ya jengo jipya la Wagonjwa wa nje wa Hospitali ya Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Meneja wa
Mradi wa Kuimarisha Afya Zanzibar (HIPZ), ambao umetoa mchango mkubwa
kufanikisha ujenzi huo, Bi. Pamela Allard akizungumza wakati wa shehere
za ufunguzi wa jengo hilo.
Naibu
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo akitoa maelezo ya ujenzi wa Jengo
hilo na baadae kumkaribisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na
Utawala Bora Dkt. Mwinyihaji Makame.(P.T)
Baadhi ya Wawakilishi wa Mashirika Wahisani wakifuatilia ufunguzi wa Jengo hilo katika Hospitali ya Kivunge.
Baadhi ya
wageni waalikwa waliohudhuria ufunguzi wa jengo la Wagonjwa wa nje
katika Hospitali ya Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, wakimskiliza
Mgeni rasmi Dkt. Mwinyihaji Makame hayupo pichani. Picha na Makame
Mshenga-Maelezo Zanzibar.
Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dkt. Mwinyihaji Makame
akizungumza na wananchi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa
Baraza la Mapinduzi wakati wa ufunguzi wa jengo la wagonjwa wa nje
liliopo Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja. Picha na Makame
Mshenga-Maelezo Zanzibar.
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema kuwa hatua za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba
za kuimarisha huduma za afya za vijijini ni miongoni mwa utekelezaji wa
shabaha ya Mapinduzi ya mwaka 1964 ya kuzifikisha huduma bora za afya
hadi vijijini kwa nia ile ile ya waasisi wa Mapinduzi.
Dk. Shein
aliyasema hayo katika hotuba yake iliyosomwa kwa niaba na Waziri wa
Nchi Afisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini,
mara baada ya kulifungua jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya
Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Katika
hotuba hiyo, Dk. Shein alisema kuwa huduma bora za afya kwa wananchi
wote bila ya ubaguzi ni miongoni mwa malengo ya Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar ya mwaka 1964 ambapo Chama cha ASP kilichoongoza Mapinduzi hayo
katika manifesto yake, kiliweka bayana azma yake ya kutoa huduma za
afya bure bila ya ubaguzi wakati kitakaposhika hatamu za Serikali.
Dk. Shein
alisema kuwa jitihada kubwa zimefanywa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi katika kuimarisha
huduma za afya kwa kutambua kwamba afya bora ni muhimu kwa wananchi ili
waweze kuishi vyema katika kazi ya kuleta maendeleo ya nchi yao.
Alisema
kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika utekelezaji wa mipango na
mikakati ya kuiendeleza sekta ya afya nchini kupitia vitengo na programu
mbali mbali zinazoendeleshwa na Serikali kwa ushirkiano na Washirika wa
Maendeleo.
“Nyote ni
mashahidi wa kuimarika kwa huduma za afya katika hospitali na vituo
vytetu vyote va afya… Aidha, kuna ongezeko kubwa la vituo vya afya vya
daraja mbali mbali kiasi kwamba hivi sasa wananchi wa Zanzibar hawawezi
kwenda zaidi ya kilomita tano bila ya kukuta kituo cha afya”,alisema Dk.
Shein.
Akieleza
historia ya huduma za afya katika Mkoa wa Kaskani Unguja, Dk. Shein
alisema kuwa kabla ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 katika Mkoa huo
kulikuwa na vituo viwili tu vya afya ambavyo vilikuwepo huko Mkokotoni
na Chaani.
Alisema
kuwa katika kipindi cha miaka 52 ya Mapinduzi Mkoa huo hivi sasa una
vituo vya afya 26 ambapo vituo 18 ni vya daraja la kwanza na 7 ni vya
daraja la pili pia, kuna hospitali ya Koteji ya Kivunge ambayo lengo la
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba ni kuipandisha daraja
kuwa hospitali ya Wilaya.
Dk. Shein
alisema kuwa lengo la mradi huo ulioanza mwaka 2012 ni kuziimarisha
huduma za afya katika hospitali zote za Koteji ili kupunguza msongamano
wa wagonjwa katika hospitali kuu ya Mnazi mmoja.
Aidha,
Dk. Shein alisema kuwa Serrikali imekusudia kuzisogeza huduma za afya
kuwa karibu zaidi na wananchi ikiwa ni pamoja na huduma za upasuaji kwa
kinamama wajawazito, huduma za uchunguzi kama vile za maabara, “X-ray”
na “Ultra-sound”.
Pamoja na
hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa shukurani za dhati kwa
Shirika lisilokuwa la Kiserikali la Uingereza HIPZ, UNICEF na ROTARY
Club kwa kuiunga mkono Serikali katika lengo la kuiimarisha hospitali
hiyo.
Dk. Shein
alisema kuwa huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo zimeimarika sana
baada ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kuongeza wafanyakazi, vifaa
vya uchunguzi wa maradhi na kuongeza aina za huduma zinzotolewa katika
hospitali hiyo.
Sambamba
na hayo, Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi juu ya umuhimu
wa kwenda kujifungulia hospitali na kuhudhuria kliniki ili kupima na
kupatiwa ushauri pamoja na kuhakikisha watoto wanapelekwa vituoni
kupatiwa chanjo kwa kuzingatia kampeni ya chankji kwa watoto
zinazoendeleshwa na Wizara ya Afya.
“Serikali
itaendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazoikabili
sekta ya afya kwa lengo la kuwapatia huduma bora za afya wananchi wote
mjini na vijijini”,alisema Dk. Shein.
Aidha,
Dk. Shein alitoa wito kwa wananchi wote kuendelea kusherehekea
maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa amani na
utulivu.
Nae Naibu
Waziri wa Wizara ya Afya Mhe. Mahmoud Thabit Kombo aliwaeleza wananchi
waliohudhuria uzinduzi wa hopaitali hiyo kuwa hatua hizo ni miongoni mwa
ahadi za Dk. Shein kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ambazo ameziahadi
na sasa anaendelea kuzitekeleza huku akitoa shukurani kwa washirika wa
maendeleo yakiwemo Mashirika ya Umoja wa Mataifa kwa kuendelea kuiunga
mkono Zanzibar.
Nae
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Mohemmed Saleh Jidawi alisema kuwa juhudi
mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa na Serikali chini ya uongozi wa Dk.
Shein katika kuhakikisha Hospitali za
kuwa za Wilaya na kueleza kuwa gharama za ujenzi huo ni milioni 461 chini ya ufadhili kutoka kwa Shirika la HIPZ.
Dk.
Jidawi alisema kuwa lengo ni kuhakikisha hospitali hiyo inakuwa ya
Wilaya na kulipongeza Shirika la HIPZ kwa kuendelea na juhudi zake
katika kuiimarisha hospitali ya Kivunge kama ilivyofanya kwa hospitali
ya Makunduchi.
Alisema
kuwa hospitali hiyo ina uwezo wa kupokea wagonjwa 120 hadi 140 kwa siku
mbapo pia hopsitali hiyo itafanya kazi kwa masaa 24 huku akieleza kuwa
hospitali hiyo inatumia mfumo wa kisasa wa kuwaorodhosha wagonjwa kwa
njia ya Kompyuta kwa lengo la kupunguza kupotea kwa kumbukumbu.
Nao
Washirika wa Maendeleo wakiwemo wawakilishi wa HIPZ, UNICEF,ROTARY CLUB
pamoja na uongozi wa Mfuko Taifa wa Bima za Afya waliahidi kuendelea
kuiunga mkono Serikali katika kuiimarisha zaidi huduma za afya hapa
nchini ikiwa ni pamoja na kukiendeleza kituo hicho cha afya ili
kitoehuduma bora kwa wananchi.
Aidha,
washirika hao walieleza kuwa kituo hicho kitakuwa ni mkombozi kwa akina
mama na kutoa shukurani kwa mashirikiano wanayoyapata kutoka kwa uongozi
wa Wizara hiyo.
Viongozi mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na mamia ya wananchi walijitokeza katika hafla hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
No comments:
Post a Comment
paulmkale