Kisa Cha Rais Aliyekatwa Masikio...!



Ndugu zangu,
Wakati mwingine kuna tunaojisahau, kuwa umri wetu umetusadia, sio tu kusoma habari za bara letu hili la Afrika na kwingineko, bali, tukiwa shule za msingi tumepata kusikia na hata kusoma habari zilizoshtusha na kubaki katika historia. Ndio , tumeshuhudia vioja pia.
Na mara nyingi Afrika husikika habari zenye kuhusiana na hazina na kilichomo kwenye hazina.
Na hiyo ndio Afrika yetu; " Ex Africa simper aliquid novi". Maana yake: "Kila kukicha kitazuka kioja kingine Afrika. Alipata kutamka Ptolemy, mwanafalsafa wa Kiyunani.
Ndio, swali kubwa Afrika ni namna gani ya kufaidika na kilichomo kwenye hazina na si namna gani ya kuongeza kilichomo kwenye hazina. Afrika mtu au kikundi cha watu wanaweza kufanya lolote lile ilimradi walifikie sanduku la hazina. Na mara nyingi mipango ya watu hao huishia hapo, huwa hawana mipango mingine kwa nchi iliyo mbele ya sanduku la hazina.
Naam, Afrika walio walio chini kabisa hawatakiwi kujua kilichomo kwenye hazina bila hizini !
Na kuna viongozi Afrika wanapenda yote; madaraka na pesa.
Kuna kisa cha Rais aliyekatwa masikio katika kugombania na wenzake, ni akina akina Prince Johnsson na Charles Taylor. Ugomvi wenyewe? Ni juu ya kilichomo kwenye hazina; mhusika mkuu ni Sajenti Samuel Doe wa Liberia.
Alfajiri ya Aprili 12, 1980, kikundi kidogo cha wanajeshi 17 kilijipenyeza ndani ya makazi ya Rais jijini Monrovia. Ikulu walimkuta Rais William Tolberts bado amelala. Wakamwua. Aliyeongoza kikundi hicho alikuwa askari kijana na wa cheo cha chini; Sajenti Samuel Doe.
Na inasemwa, kuwa Doe alipoingia Ikulu na wenzake alidhani watakwenda kumlalamikia Rais juu ya mishahara midogo ya askari wa vyeo vya chini. Lakini, jinsi walivyoikuta Ikulu ikiwa nyepesi vile, ndivyo mipango ilipobadilika na kufanya maamuzi ya kumwua Rais mwenyewe , na hivyo, kuchukua madaraka.
Naam, Samuel Doe alikuwa askari ambaye hata madarasa manne ya shule ya msingi hakuyamaliza. Alitoka kabila dogo la waishio misituni. Kabila la Krahn. Ni watu wa kabila kama lake, masikini na ambao ndio waliotoka vijijini na kukimbilia jijini Monrovia kutafuta vibarua na pesa. Kwa wenye bahati, kama Samuel Doe, walionekana mitaani na kuitwa kujiunga na Jeshi.
Vinginevyo, wengi wa vijana hawa hawakuwa na cha kufanya mijini. Hawakuwa na kazi. Na idadi yao iliongezeka. Na si Monrovia tu, ni katika miji mingine ya Afrika. Hali hiyo imeendelea hata leo hii. Na sasa hali ni mbaya zaidi.
Tangu siku ya kwanza, Afrika kijana anayeingia mjini na kuishi bila kazi hugeuka kuwa bayaye. Ndivyo walivyokuwa wakijulikana katika nchi ya Uganda. Na miji mingi ya Afrika ya sasa imefurika ma-bayaye. Ni jeshi la wasio na kazi- ni bomu linalosubiri wakati kulipuka.
Sajenti Samuel Doe naye alikuwa bayaye, ni kama ilivyokuwa kwa Idi Amin wa Uganda. Na kama ilivyokuwa kwa Idi Amin, Urais ulimdondokea tu Samuel Doe- kama vile mtu aliyeshinda bahati nasibu.
Ujio wa Samuel Doe uliwafanya WaLiberia waamini kuwepo kwa mabadiliko. Kuondokana na utawala wa kifisadi na kirasimu wa William Tolberts.
Samuel Doe akajitangaza kuwa Rais. Haraka sana akawatwanga risasi mawaziri wote wa Tollberts. Ni kwenye pwani ya bahari huku wananchi wakitazama kama mechi ya mpira.
Sajenti Samuel Doe akatawala kwa kipindi cha miaka kumi. Nchi ikawa kama imesimama.
Sajenti Samuel Doe alibaki madarakani Liberia kwa miaka kumi. Nchi ilikuwa kama imesimama vile. Sehemu kubwa ya nchi haikuwa na umeme. Maduka mengi hayakuwa na bidhaa.
Doe mwenyewe alinusurika majaribio takribani 34 ya kutaka kumwua. Na wote waliojaribu kumwua wakashindwa waliishia kupigwa risasi.
Kwamba alinusurika majaribio 35 ikasemwa kuwa Sajenti Samuel Doe alikuwa akilindwa na ’ nguvu’ za kishirikina. Na Doe mwenyewe alikuwa akitamba hadharani kuwa ni ’ mjanja’ kwenye mambo hayo.
Kimsingi Samuel Doe aliingia Ikulu lakini hakujua afanye nini kama Rais.
Na kwa vile Doe alikuwa na sura ya kitoto alipenda sana kuvaa miwani ya jua ya mviringo ili aonekane ’ siriaz’ fulani. Na kwa vile cheo cha sajenti ni cheo cha chini sana jeshini, Samuel Doe akajipa cheo cha ' 'Master Seargent'
Vinginevyo, Sajenti Samuel Doe alikuwa Rais mvivu sana. Muda mwingi aliutumia akiwa Ikulu akicheza bao na wasaidizi wake. Na mara nyingine alionekana kwenye bustani ya Ikulu akipunga hewa huku wake zake wakimpikia chakula kwenye moto wa kuni kwenye majiko ya mafiga . Alipenda chakula kipikwe kama ilivyokuwa kijijini kwao alikokulia.
Kwa vile Sajenti Samuel Doe alishawaua watu wengi, naye akawa ni mwenye mashaka sana. Alihofia wengine kulipiza kisasi juu yake. Hakujua hasa cha kufanya. Hakuwaamini watu wasio wa karibu yake na hususan watu wa kabila lake, krahn.
Watu wengi wa kabila lake walikusanyika jijini Monrovia na walionekana ghafla, kuwa ndio wenye fursa zaidi kutoka kwenye hali ya umasikini mkubwa. Hao ndio watu ambao Samuel Doe aliweza kujumuika nao na aliwasaidia.
Na watu wa kabila la Samuel Doe waliogopewa na makabila mengine. Waliweza kufanya lolote lile na hakuna aliyewagusa. Waliua na waliwatisha wengine. Wengi wasio wa kabila la Doe waliishi kwa hofu kubwa.
Na kile ambacho kila mtu, asiye wa kabila la doe, alikuwa anakisubiri, ni kushuhudia mwisho wa Sajenti Samuel Doe.
Na hapa akatokea Charles Taylor. Huyu alikuwa rafiki wa zamani wa Sajenti Samuel Doe.
Lakini, urafiki wao ulikufa pale Samuel Doe alipodai kuwa Charles Taylor alimtapeli Doe dola milioni moja. Kisha Taylor akatorokea Marekani. Huko akaanza kufanya biashara kwa mtaji wa fedha alizomtapeli Sajenti Samuel Doe.
Charles Taylor nae akaishia gerezani nchini Marekani kwa mashtaka ya utapeli. Lakini, akatoroka jela na kukimbilia Ivory Coast. Na akiwa Ivory Coast, Charles Taylor akaanza kujipanga kwenda kuuangusha utawala wa Sajenti Samuel Doe.
Ndugu zangu, ngoja na leo niishie hapa....

No comments:

Post a Comment

paulmkale