Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein
amesema yeye bado ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na kutoa changamoto kwa
wasioiamini Katiba hiyo kupeleka shauri hilo Mahkama Kuu ya Zanzibar
ambayo ndiyo pekee yenye uwezo wa kutafsiri Katiba.
Amebainisha
kuwa yeye anaongoza nchi kwa mujibu wa Katiba na Sheria na kwamba kama
si uwezo huo aliopewa Kikatiba hana sababu ya kuendelea kukaa madarakani
pamoja na serikali anayoingoza.
“Tuko
madarakani na uongozi wote wa serikali... yupo Makamu wa Kwanza wa Rais,
Makamu wa Pili wa Rais na mawaziri” alisisitiza Dk. Shein na kuongeza
kuwa hao wanaodai kujiondoa serikalini huo ni uamuzi wao wenyewe.
Alibainisha
kuwa yeye na serikali anayoingoza kuendelea kuwepo madarakani “si
uamuzi wake” na wala yeye hana “ubavu” wa kujiweka madarakani bali ni
Katiba ambayo inajieleza wazi.
Dk. Shein
ametoa kauli hiyo leo kwa nyakati tofauti wakati alipokuwa akizungumza
na wananchi wa Mkoa wa Kusini Pemba katika siku yake ya kwanza ya ziara
yake ya siku tatu kisiwani humu kukagua na kuzindua miradi ya maendeleo
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.
Aliwaambia
wananchi hao kuwa yako mengi yanayosemwa lakini hawapaswi kuyasikiliza
kwa kuwa kama ni serikali yeye ndiye Rais hivyo wanapaswa kumuamini
anachowaeleza.
“Ya mjini
yapo yasikilizeni lakini kwa Serikali mimi ndiye Rais na nisiposema
mimi nitawatuma wasaidizi wangu kuwaeleza” Dk. Shein alibaisha na
kuongeza kuwa ya vyama kila mtu ana chama chake.(P.T)
Alifafanua
kuwa kama ni suala la Chama cha Mapinduzi (CCM) yeye ndiye Makamu
Mwenyekiti Zanzibar na kama kuna la kuwaeleza wana CCM na wananchi
atawaeleza yeye na viongozi wenzake wa chama hicho pamoja na taarifa za
vikao vya chama vyake.
Dk. Shein
aliwaeleza wananchi hao kuwa ushindani wa kisiasa si ugomvi bali ni
utaratibu wa kupeana changamoto katika uongozi ambao lengo ni kuwaletea
wananchi maendeleo.
“tusikejeli maendeleo yetu, tuthamini chetu na ushindani wetu wa kisiasa usirejeshe nyuma maendeleo yetu” Dk. Shein alitahadharisha.
“tusikejeli maendeleo yetu, tuthamini chetu na ushindani wetu wa kisiasa usirejeshe nyuma maendeleo yetu” Dk. Shein alitahadharisha.
Dk. Shein
aliruejea wito wake wa kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika
maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yameanza tarehe 3
Januari na yanatarajiwa kufikia kilele tarehe 12 Januari, 2016 katika
kiwanja cha Amaan.
Aliwakumbusha
wananchi hao kuwa Mapinduzi ya Zanzibar ambayo yaliyomfanya Rais wa
kwanza wa Zanzibar Mzee Abeid Amani Karume kutangaza Jamhuri ya
Zanzibar, ndiyo yaliyowakomboa wanyonge wa Visiwa vya Zanzibar kwa
kuondosha aina zote za ubaguzi na kuwapa mamlaka ya kujiamulia mambo
yao.
Dk. Shein
aliwaeleza wananchi wa Pemba kuwa meli mpya iliyonunuliwa na Serikali
MV Mapinduzi II ambayo ilizinduliwa hivi karibuni, itawasili kisiwani
humo tarehe 10 Janauri na siku itakayofuata itawachukua baadhi ya
wananchi kwenda Unguja kushiriki maaadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi.
Alisisitiza
kuwa serikali itawalipia gharama za usafiri wa kwenda na kurudi Unguja
wale wote watakaoteuliwa kuwemo kwenye safari hiyo kufuatana na
utaratibu utakaowekwa kama alivyokuwa ameahidi wakati meli hiyo
ilipokuwa inatengenezwa nchini Korea ya Kusini.
Katika ziara hiyo Mheshimiwa Rais amefuatana na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wabunge.
No comments:
Post a Comment
paulmkale