Mfalme wa Saudi Salma bin Abdul-Aziz al-Saud.
Saudi
Arabia imevunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran, baada ya waandamanaji
kuuvamia ubalozi wake mjini Tehran na kuuchoma moto, na kutoa saa 48 kwa
wanadiplomasia wa Iran kuondoa nchini humo.
Hatua ya
Saudi Arabia ilikuja saa chache baada ya waandamanaji kuuvamia na
kuuchoma moto ubalozi wake mjini Tehran, katika kupinga mauaji ya
kiongozi wa Kishia Sheikh Nimr al-Nimr.
Mauaji ya
Nimr pamoja na wengine 46 - ambayo ndiyo makubwa zaidi kufanywa kwa
wakati mmoja katika kipindi cha miongo mitatu na nusu - yamebainisha
wazi migawanyiko mikubwa inayoikabili kanda ya Mashariki ya Kati, ambako
waandamanaji waliingia mitaani kuanzia Bahrain hadi Pakistan kuyapinga.
Al-Nimr
alikuwa mtu muhimu katika maandamano ya Washia wachache wa Saudi Arabia,
yaliyohamasishwa na uasi wa umma katika mataifa kadhaa ya Kiarabu, hadi
alipokamatwa mwaka 2012.
Alitiwa
hatiani kwa makosa ya ugaidi, lakini alikanusha kuchochea vurugu.
Kiongozi wa juu kabisa nchini Iran, Ayatollah Ali Khomenei, alisema
Saudi Arabia italipa gharama kubwa kwa mauaji ya Nimr.
Aituhumu Tehran kwa kuendeleza sera za kibabe.(P.T)
Waziri
al-Jubeir alisema mashambulizi dhidi ya balozi zake nchini Iran ni
mwendelezo wa sera za kibabe za utawala wa Tehran katika kanda hiyo,
zinazolenga kuvuruga usalama na kueneza ugomvi na vita, ambavyo amesema
vinathibitishwa na hatua ya Iran kuwapa hifadhi viongozi wa Al-Qaeda
tangu mwaka 2011, na pia kuwapatia ulinzi baadhi ya walioshiriki katika
uripuaji wa majengo ya al-Khobar mwaka 1996.
"Kwa
kuzingatia ukweli huu, Saudi Arabia inatangaza kuvunja uhusiano wa
kidiplomasia na Iran, na inaomba kwamba wanadiplomasia wote walioko
ubalozini, ubalozi mdogo na ofisi tanzu zote kuondoka katika muda wa saa
48," alisema Al-Jubeir.
Iran
ilisema iliwakamata watu 44 kuhusiana na mashambulizi ya ubalozi, na
rais Hassan Rouhani akawaelezea waandamanaji hao kuwa wenye itikadi
kali, na kwamba mashambulizi dhidi ya balozi za Saudi hayakuwa na
uhalali wowote.
Visasi vyaanza
Nchini
Iraq, misikiti miwili ya Kisunni imeripotiwa kushambuliwa kwa mabomu
katika mkoa wa katikati mwa nchi hiyo wa Hilla, huku muadhini akiuawa
kwa kupigwa risasi karibu na nyumbani kwake mjini Iskandariya, kulingana
na maafisa wa polisi na wahudumu wa afya.
Katika
mkoa huo wa Hilla, uliyoko umbali wa kilomita 80 kusini mwa mji mkuu
Baghdad, Afisa wa polisi alisema msikiti wa Ammar bin Yasser uliyoko
katika kijiji cha Bakerli uliripuriwa kwa mabomu usiku wa manane.
"Baada ya
kusikia mripuko, tulienda mahala ulipotokea na kukuta vifa vya miripuko
vya kutengeneza kienyeji vikiwa vimewekwa katika msikiti, alisema
kapteni huyo wa polisi. "Wakazi walisema watu waliovalia sare za jeshi
walifanya operesheni hiyo," alisema na kuongeza kuwa nyumba 10
ziliharibiwa katika mripuko huo.
'Saudi yafunika makosa yake'
Naibu
waziri wa mambo ya nje Hossein Amir Abdollahian alinukuliwa akisema
uamuzi wa Saudi kuvunja uhusiano na Iran hauwezi kuifanya dunia isahau
kosa lake kubwa la kumuua Nimr.
"Kwa
kuamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia, Saudi Arabia haiwezi kuifanya
dunia isahau kosa lake kubwa la kumuuwa," alisema naibu waziri huyo
akinukuliwa na shirika la habari la Iran IRNA.
Aliongeza
kuwa Saudi Arabia ilifanya kosa la kimkakati kwa kuchukuwa maamuzi ya
haraka, ambayo yameeneza ukosefu wa utulivu na kusababisha kukuwa kwa
ugaidi katika kanda.
Naye
msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Hossein Jaberi Ansari, alisema
katika matamshi yaliyotangazwa kwenye televisheni, kuwa Iran inayo
dhamira ya kuzilinda balozi zote za kigeni chini ya mikataba ya
kimataifa. Lakini ailiongeza kuwa Saudi Arabia imetumia tukio hilo kama
kisingizio cha kuchochea mgogoro.
Uhusiano wa mivutuno
Uhusiano
kati ya Saudi Arabia na Iran umekuwa wa mivutano kwa miongozo kadhaa,
huku Riadh ikiishtumu Tehran mara kwa mara kwa kuingilia masuala ya
mataifa ya Kiarabu.
Mataifa
hayo mawili pia yamegawanyika juu ya vita vya karibu miaka mitano nchini
Syria, ambako Iran inaunga mkono utawala wa Bashar Al-Assad, na katika
mgogoro wa Yemen ambako muungano unaongozwa na Saudi Arabia unapambana
dhidi ya waasi wa Kishia.
Abdollahian
ameituhumu pia Saudi Arabia kwa kile alichokiita "kupuuza maslahi ya
watu wake na Wasilamu wa kanda hiyo kwa njama yake ya kushusha bei za
mafuta," akimaanisha bei za mafuta ghafi ambazo ziko karibu kufikia
kiwango cha chini kabisa kuwahi kushuhudia katika kipindi cha miaka
kadhaa.
No comments:
Post a Comment
paulmkale