TRA YAONGEZA MWEZI MMOJA USAJILI WA PIKIPIKI

Na Raymond Mushumbusi MAELEZO
Mamlaka ya Mapato ya Tanzania (TRA) imesema imeongeza muda kwa usajili wa vyombo vya usafiri vya Pikipiki za magurudumu mawili na matatu mpaka Februari Mosi mwaka 2016.
Hayo yamesemwa leo na Kaimu Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo Alphayo Kidata alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari katika kikao chake cha kutoa taarifa kwa umma juu ya ukusanyaji wa kodi, Kaimu Kamishna Mkuu amesema wameamua kuongeza muda wa zoezi la usajili wa pikipiki ili kuiwapa nafasi wale ambao bado hawajasajili.
“ Natoa wito kwa wamiliki wa vyombo vya pikipiki kusajili vyombo vyao mapema ili wasipatwe na adha itakayojitokeza baada ya muda uliotolewa kumalizika ” Alisema Kaimu Kamishna Kidata.
Ameongeza kuwa zoezi hilo lilikumbwa na changamoto kadhaa zilizowalazimu kuongeza muda mara mbili, ambazo ni umbali wa vituo vya usajili na makazi ya wamiliki wa pikipiki hasa mikoani,pamoja na upotevu wa nyaraka za kununulia pikipiki.
Aidha Kaimu Kamishna Alphayo Kidata ameomba wananchi kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano na Mamlaka ili kutimiza azimio la Serikali ya Awamu ya Tano ya kulijenga taifa kwa kufanya kazi na hasa kulipa kodi stahiki zinazoleta mapato yanayowezesha maendeleo katika taifa letu.
Zoezi la usajili wa pikipiki lilianzishwa kwa lengo la kurahisisha ukusanyaji wa mapato kutoka katika vyombo hivyo, zoezi hili lilipangwa kukamilika tangu Desemba 31 2015 lakini ikaonekana wengi hawakusajili pikipiki zao hivyo basi Mamlaka imetoa mwezi mmoja mpaka Februari Mosi 2016 kwa wenye Pikipiki kusajili.

No comments:

Post a Comment

paulmkale