TAARIFA KWA UMMA
Kumekuwa na
upotoshwaji kuhusu zoezi la ufuatiliaji wa matumizi ya misamaha ya kodi
inayosimamiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa wafanyabiashara,
wawekezaji, Taasisi za Dini na Taasisi zisizo za kiserikali kwa maelezo
kwamba TRA inazilenga baadhi ya Taasisi.
Sheria ya Mamlaka ya
Mapato Tanzania inaipa Mamlaka ya kusimamia, kukagua na kuhakiki mapato
ya Serikali pamoja na kuzuia ukwepaji wa kodi wa aina yoyote ile ikiwemo
matumizi mabaya ya misamaha ya kodi inayotolewa kwa mujibu wa Sheria.
Kifungu
cha 5 (3) cha Sheria ya TRA kinatoa mamlaka kwa TRA kufanya jambo
lolote lenye tija na manufaa katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu
yake kisheria.
Kwa vile misamaha ya kodi inatolewa kwa mujibu wa
Sheria zinazosimamiwa na TRA, ni wajibu wa Mamlaka kuhakiki kama bidhaa
au huduma zilizosamehewa zinatumiwa na watu au Taasisi zinazostahiki
misamaha hiyo au kwa miradi iliyokusudiwa.
Hivi karibuni
kumekuwepo na taarifa za upotoshaji kwamba TRA imeilenga Taasisi moja ya
kidini kwa kuiandikia barua ya kuomba vielelezo na ufafanuzi juu ya
misamaha ya magari iliyopewa awali na kuonekana kana kwamba ni utaratibu
mpya wa utoaji wa misamaha.
Tungependa kufafanua kwamba TRA
haibagui wala kulenga Taasisi yoyote bali inatekeleza wajibu wake wa
kufuatilia misamaha iliyotolewa
Katika kipindi cha Mwezi Oktoba
hadi Desemba 2015 TRA iliwaandikia walipakodi 65 kupata vielelezo juu ya
matumizi ya misamaha ya kodi walioipata na katika hao zimo Taasisi za
kidini 39.
Ukaguzi huu huisadia TRA kupata taarifa muhimu ili
kuishauri Serikali namna bora ya kutoa misamaha kwa ajili ya kuleta tija
na ufanisi uliokusudiwa ikiwemo kurahisisha upatikanaji wa huduma
muhimu za jamii na kupunguza umaskini.
Aidha taarifa za misamaha
ya kodi zinaisadia TRA kubaini matumizi bora ya misamaha pamoja na
mianya ya upotevu wa mapato kupitia misamaha hiyo ili TRA ichukue hatua
zinazostahili pale inapobainika kuwa kuna ukwepaji na kuziba mianya
hiyo.
Zoezi hili ni endelevu hivyo tunaziomba Taasisi zote za
kidini na mashirika yote yanayonufaika na misamaha ya kodi kuchukulia
zoezi la ukaguzi wa misamaha hiyo kuwa ni utekelezaji wa sheria na
wahusika wote watoe ushirikiano kwa TRA pale wanapohitajika ili zoezi
hilo lifanyike kwa ufasaha na kwa manufaa kwa wote.
"Pamoja Tunajenga Taifa Letu"
A. J. Kidata
KAIMU KAMISHNA MKUU.
No comments:
Post a Comment
paulmkale