Balaa la majeruhi Man United laendelea.
Mkosi wa majeraha umeendelea kuiandama Manchester United baada ya
kushuhudia wachezaji wake wawili wakiumia hapo jana ukiwa ni muendelezo
wa majeraha ambayo yamekuwa yakiwaandama wachezaji wa Manchester United
karibu msimu mzima .
Katika mchezo wa raundi ya tatu ya kombe la FA dhidi ya timu ya
Yeovil Town kocha Louis Van Gaal aliwashuhudia mabeki wa pembeni Rafael
Da Silva na Luke Shaw wakitoka nje huku wakiwa na majeraha yanayohofiwa
kuwa ya muda mrefu .
Beki wa kulia raia wa Brazil Rafael Da Silva alipata jeraha baya
ambalo linaaminika kuwa la kuvunjika kwa mfupa wa taya baada ya
kugongana vichwa na mchezjai wa Yeovil wakati wa kuwania mpira wa juu .
Beki mwingine wa kushoto Luke Shaw aliumia kifundo cha mguu wake
baada ya kuwa anacheza kwa maumivu kwa muda mrefu na baada ya kushindwa
kuvumilia alilazimika kutoka uwanjani.
Majeraha haya yanafuatia majeraha ambayo yalitokea kwa Ashley Young
na Antonio Valencia walioumia kwenye mchezo dhidi ya Tottenham Hotspurs
huku Marouanne Fellaini akiumia kwenye mazoezi kabla ya mchezo huo .
United bado inaendelea kuwakosa wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza
kutokana na majeruhi akiwemo kiungo Mholanzi Daley Blind na beki
Muargentina Marcos Rojo.
No comments:
Post a Comment
paulmkale