Yanga Vs Mbeya City Kikosi cha kwanza Yanga hiki hapa

YANGA imeendelea kuonyesha kuwa haitaki utani katika msimu huu wa 2015/16, hiyo ni kutokana na mazoezi ambayo timu hiyo imekuwa ikiyafanya lakini zaidi ni kuwa kikosi cha kwanza kipo kamili.

Yanga itakutana na Mbeya City, kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar katika mchezo wa Ligi Kuu Bara lakini tayari Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameshapata kikosi kitakachocheza mchezo huo na mbadala wa wale ambao watapata matatizo au kuwa nje ya uwanja kwa sababu yoyote ile.

Katika mazoezi ya jana asubuhi kwenye Uwanja wa Boko, Beach Veteran nje kidogo ya Dar, kocha huyo alipanga vikosi viwili na kucheza kama mechi kati ya hivyo vyote kilikuwepo kimoja alichoonekana akikiandaa zaidi kwa kukipa mbinu nyingi.

Kikosi kinachoaminika kuwa ni cha kwanza na kitaanza katika mchezo wa kesho kiliundwa na; Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Vincent Bossou, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite, Deus Kaseke, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Simon Msuva.

Kikosi cha pili ambacho ni wazi kinaweza kuwa mbadala wa nafasi za wale waliopo kwenye kikosi cha kwanza kiliundwa na; Benedicto Tinoko, Oscar Joshua, Salum Telela, Pato Ngonyani, Hassani Mwakipa, Juma Makapu, Geofrey Mwashiuya, Malimi Busungu, Paul Nonga, Matheo Anthony na Boubacar Garba.

Ikiwa kikosi cha kwanza kitapangwa hivyo maana yake ni kuwa, Msuva na Kaseke ambao walikuwa wakipata nafasi katika kikosi cha kwanza kimachale, watakuwa wamechukua nafasi ya Busungu aliyekuwa akipangwa kushambulia akitokea pembeni.

Upande wa wachezaji wapya waliotua hivi karibuni, Nonga na Boubacar bado wanahitaji muda ili kocha awaone na kuna uwezekano wakaingia wakitokea benchi katika mchezo huo.

Katika mazoezi hayo, Pluijm alikuwa akiwataka wachezaji wake kucheza soka la pasi za haraka, huku Ngoma na Kamusoko wakionekana kivutio kutokana na aina ya soka lao kuwafurahisha waliojitokeza uwanjani hapo.

Kuhusu mchezo huo wa kesho, Pluijm alisema: “Maandalizi ya kikosi changu yanaendelea vizuri na tunachosubiri ni ushindi tu.

“Katika mazoezi ya leo kama ulivyoona, nilikuwa nikisisitiza wachezaji wangu kucheza soka la pasi za haraka wakati tukiwa na mpira tunashambulia goli la wapinzani, hiyo yote ni katika kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.”

No comments:

Post a Comment

paulmkale