Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe ametoa mwelekeo wa upangaji wa uongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni na baraza kivuli la mawaziri, huku akionyesha kambi hiyo kuwa tayari kushirikiana na Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.
Akizungumza
jana mjini Dodoma Mbowe alisema idadi ya wizara hizo itafanana na ya
wizara za Serikali ya Awamu ya Tano ambazo zipo 19.
“Tutatangaza
baraza kivuli kabla ya kumalizika kwa mkutano wa Bunge Ijumaa wiki hii
na baraza hili litashirikisha vyama vyote vinavyounda Ukawa,” alisema Mbowe.
Alisema
kigezo cha kwanza kitakuwa uzoefu na taaluma za wabunge kikifuatiwa na
mgawanyo wa nafasi kwa kuzingatia kipaumbele hicho kwanza.
“Tutazipanga
kulingana na muundo wa Muungano kwa sababu kuna wizara ambazo ni sehemu
ya Muungano. Nne tutazingatia jinsia kadri iwezekanavyo na tano
tutazingatia uteuzi kulingana na mikoa, yaani mawaziri vivuli
watateuliwa kulingana na mikoa wanayotoka kadri itakavyowezekana.”
Alisema
miaka yote, upinzani ulikuwa ukiitaka Serikali kupunguza ukubwa wa
Baraza la Mawaziri, hivyo uamuzi wa Rais John Magufuli kupunguza idadi
ya wizara ni jambo zuri na wao watafanya hivyo katika uteuzi wa baraza
hilo kivuli.
Kuhusu Zitto alisema:
“Katika siasa na ushirikiano wa vyama hakuna mazingira ya kudumu. Jambo
lolote linawezekana lakini kuna taratibu zake na muda ndiyo huwa
unaongea.”
Alisema
Chadema na NCCR vimewahi kuwa na wabunge ambao kwa sasa ni makada wa
CCM, huku akitolea mfano jinsi Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa
alivyohama CCM na kujiunga na Chadema na kugombea urais.
“Hatujawahi
kama kambi ya upinzani kumtenga Zitto kwenye kila jambo, yapo mambo
tunaweza kulazimika kutengeneza ushirikiano na wabunge hata wa CCM ili
kufanya jambo fulani kutekelezeka.
“Kushirikiana
na Zitto si jambo la ajabu kama ambavyo umeona tukilifanya. Yapo
majeraha mengi ambayo tumeyapitia pande zote (Chadema na Zitto) ambayo
huwezi kuyatibu kwa siku moja.
"Yapo
ambayo yatapona kulingana na muda. Unaweza kumfanyia mtu kitu kibaya,
lakini baadaye ukatambua kuwa umekosea. Chochote katika siasa
kinawezekana,” alisema Mbowe.
Zitto
alifukuzwa Chadema na kujiunga na ACT Wazalendo Machi 21, 2015 chama
ambacho hakina ushirikiano na vyama vinavyounda Ukawa lakini katika siku
za karibuni ameonekana kuwa karibu na umoja huo wa wananchi, ikiwa ni
pamoja na kushirikiana kuibua hoja mbalimbali katika mkutano wa Bunge
unaoendelea mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment
paulmkale