Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu amesema ununuzi wa ndege za
Bombardier uliofanywa na Serikali hauna tija kwa wananchi wa jimbo lake
iwapo huduma za afya na barabara hazijaboreshwa.
Kadutu ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 20, 2018 katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2018/19 bungeni mjini Dodoma.
Amesema umebaki mwaka mmoja kabla ya nchi kuingia katika Uchaguzi Mkuu
wa mwaka 2020, hivyo ahadi zilizotolewa zinapaswa kutekelezwa.
“Serikali imejenga reli, inanunua ndege hebu twendeni kwa wananchi, ujue
ukienda kule Ulyankulu ukauliza Bombardier hawakuelwi, barabara mbovu,
afya mbovu hawakuelewi,” amesema Kadutu.
“Pelekeni fedha barabara ziboreshwe, Tarura (Wakala wa Barabara Mijini
na Vijijini) wapewe fedha. Bajeti iliyobaki ni moja ya kujadili kwa
utulivu kwani akili itakuwa majimboni tu, tusaidieni ili mwaka 2020
tupete,” amesema.
Akigusia ahadi za kampeni za uchaguzi, Kadutu amesema waliahidiwa jimbo
la Ulyankulu litakuwa wilaya lakini mpaka sasa ahadi hiyo
haijatekelezwa.
“Hamtaki kutupa eneo lakini mnasema ahadi za Rais zitatekelezwa, sasa
hii ni ahadi ya Rais, alisema akiingia siku tatu tu tunapata wilaya,”
amesema.
“Sasa imebaki mwaka mmoja tu na nusu yako mengi, mmetuahidi lami tena
kilomita tatu tu lakini tunaona mambo ambayo hayako katika ilani
yanatekelezwa. Tukisema…,mimi watu wa Ulyankulu wamenituma.”
Mbunge huyo amesema anashangazwa na mawaziri kutotembelea jimboni kwake
huku wakionekana kupishana katika majimbo mengine jambo linalokatisha
tamaa wananchi.
No comments:
Post a Comment
paulmkale