Wabunge Waibua UFISADI Mradi wa Stempu za Kielekroniki

Bunge limeitaka serikali kujiridhisha kuhusu gharama za mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki huenda ukamnufaisha zaidi mwekezaji wa kigeni, huku ukiongeza gharama kwa watumiaji wa vinywaji nchini.

Limesema limebaini udhaifu katika makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo kwa kuwa linaona gharama zitabebwa na watumiaji wa bidhaa (soda, juisi, maji na bia).

Udhaifu katika makubaliano hayo uliibuliwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Hawa Ghasia, alipowasilisha bungeni jijini Dodoma jana taarifa ya kamati yake kuhusu mapendekezo ya bajeti ya serikali kwa mwaka ujao wa fedha na Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2017.

Vilevile, baadhi ya wabunge waliochangia bungeni jana kuhusu mapendekezo hayo ya serikali, walishauri kupitiwa upya kwa gharama za utekelezaji wa mradi huo, wakidai zimekuwa mara 10 ya nchi nyingine zinazoutumia.

Katika taarifa yake, Ghasia alisema katika mwaka ujao wa fedha, serikali imedhamiria kuanzisha mfumo wa stempu za kodi za kielektroniki ili kudhibiti udanganyifu wa wazalishaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru wa bidhaa.

Alisema kampuni ya SCIPA kutoka Uswisi ndiyo iliyoshinda zabuni hiyo na ina mkataba wa miaka mitano na serikali kwa mfumo wa 'Self Financing'.

Alisema mfumo huo unamtaka mwekezaji kurudisha gharama zake za uwekezaji kwa kutoza stempu ya kielektroniki kwa kila bidhaa itakayozalishwa na kwamba kiasi cha fedha kinachotarajiwa kuwekezwa na SCIPA ni Dola za Marekeni 21,533,827 (Sh. bilioni 48.473).

"Kamati haina pingamizi na uanzishwaji wa mfumo huu, jambo la msingi ambalo linahitaji lifanyike kwa umakini ni kujiridhisha na gharama za mfumo huo, ambazo zitabebwa na watumiaji wa bidhaa pamoja na mapato atakayoyapata mwekezaji kutokana na stempu," Ghasia alisema.

"Kamati ina maoni kuwa hatua ya serikali kutoongeza ushuru wa bidhaa zisizo za petroli itakuwa haina maana kama gharama ya stempu itabaki kama ilivyopangwa na serikali. Hatua hii itasababisha kuongezeka kwa bei kwenye vinywaji kama maji, soda, bia na juisi ambazo sasa hazitozwi stempu.

"Tathmini ya kamati inaonyesha kuwa pale serikali itakapokuwa inaongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia ya mfumuko wa bei kama Sheria ya Ushuru wa Bidhaa inavyotaka, kiwango cha stempu kitakuwa kinaongezwa juu yake kulingana na mkataba kwa miaka

mitano," alisema.

Ghasia ambaye pia ni Mbunge wa Mtwara Vijijini (CCM), alisema kamati yake imefanya uchambuzi ili kubaini kiwango cha fedha ambacho kampuni ya SCIPA itakipata katika mkataba huo kwa mwaka mmoja.

Alisema uchambuzi wao ulihusisha takwimu za bidhaa tatu za maji, soda na sigara bila spiriti kwa kuangalia viwango vya uzalishaji wa bidhaa hizo kwa mwaka.

Alisema uzalishaji huo unaonyesha kiwango cha maji kinachozalishwa nchini kwa mwaka ni lita za ujazo 268,702,209, soda lita 732,315,008, bia lita 409,274,746 na sigara ni pakti 429,310,400.

"Mheshimiwa Spika, ukikadiria kwamba stempu itatozwa kwa idadi (unit) na si kwa ujazo (lita), hivyo chupa moja ya bia mls 500 itatozwa Sh. 22.73; soda 500 mls itatozwa Sh. 13.5, spiriti mils 1,000 itatozwa Sh. 29.57," alisema.

"Hivyo, ukijumlisha na ushuru wa bidhaa kwa kila bidhaa iliyoainishwa hapo juu, inaonekana kuwa gharama itakwenda kwa mlaji wa mwisho.

"Kwa mantiki hii, ukokotoaji unaonyesha kwa mwaka mmoja SCIPA atakusanya jumla ya Sh. bilioni 66.69 bila ya kuhusisha takwimu za bidhaa ya spiriti. Kiasi hiki ni kikubwa kuliko alichowekeza katika kipindi cha mwaka mmoja tu wa mkataba.

"Kamati imekuwa ikifuatilia hatua mbalimbali za serikali zenye lengo la kukusanya mapato yake yenyewe na sio kutumia mawakala kukusanya mapato.

"Mfano; kuhamisha fedha zake kutoka Benki Binafsi kupeleka Benki Kuu, mfumo wa manunuzi ya Luku kutoka Kampuni ya MaxMalipo na Mitandao ya simu kwenda GePGS (Government Electronic Payment Gateway System), ukusanyaji wa mapato katika mabasi ya mwendo kasi na matumizi ya mashine za EFD.

"Kamati inaona kuwa serikali kuamua kumpa SCIPA mkataba wa miaka mitano wa kuhakiki uzalishaji kupitia stempu za kielektroniki ilhali uhakiki huu ungeweza kufanywa na serikali yenyewe.

"Hata hivyo, kamati imeona kuwa kiwango cha mapato kinachotarajiwa kukusanywa katika kipindi cha mwaka mmoja (Sh. bilioni 66.69) kwa bidhaa nne zilizoainishwa hapo juu ni kikubwa kuliko kiwango cha uwekezaji cha Sh. bilioni 48.473 ambacho kimewekezwa na Kampuni ya SCIPA."

Ghasia alisema baada ya kamati kufanya uchambuzi huo, inaishauri serikali iwekeze yenyewe mfumo huo wenye mtaji wa kiasi cha Sh. bilioni 48.473, ili kiasi cha fedha kitakachopatikana kiwe ni sehemu ya mapato ya serikali badala ya mapato yatokanayo na stempu kuchukuliwa na kampuni binafsi kama ilivyofanya kwenye Mfumo wa TANCIS.

Vilevile, alisema wanaishauri serikali ianze kutumia mfumo huo kwenye vinywaji vikali ambavyo mara kwa mara mbele ya kamati hiyo serikali imekuwa ikithibitisha kuna udanganyifu mkubwa.

"Ni bora serikali kuongeza ushuru wa bidhaa kwa asilimia tano ya mfumuko wa bei kama ilivyokuwa ikifanya hapo awali kuliko inavyopendekeza sasa kutumia mfumo wa stempu kwa bidhaa hizo kwa kuwa gharama za stempu ni kubwa kuliko ushuru wa bidhaa wa asilimia tano," Ghasia alisema na kufafanua zaidi:

"Mathalani ukichukua bidhaa ya soda (Mils 250) inatozwa ushuru wa bidhaa kiasi cha Sh. 15 na wa stempu utatozwa kiasi cha Sh. 13.5. Hivyo, gharama ya jumla (gharama ya ushuru wa bidhaa na wa stempu) itakuwa kiasi cha 28.5 na hivyo itaongeza gharama kwa uzalishaji na kwa mlaji."

Akichangia mjadala huo jana, Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu (CCM), alidai kampuni iliyopewa tenda ya mfumo huo ina matatizo makubwa na imeziangusha serikali zingine kutokana na mfumo wake wa rushwa.

“Hili la stempu za kielektroniki ni jambo zuri, lakini tumechelewa," Zungu alisema, "nilitaka kujiridhisha serikali imejiridhisha na huyu aliyepewa kazi hii kwa sababu ukitazama taarifa mbalimbali ina matatizo makubwa, ina kesi Morocco wamefanya ‘price offering’ mara 10 zaidi ya nchi zingine walizofanya kazi hii.

“Kampuni hii inachunguzwa na Bunge la Kenya na imeziangusha serikali zingine kutokana na mfumo wake wa rushwa. Napenda waitwe hawa mabalozi waliopitisha hii kampuni kwamba taarifa zao walizipata wapi.

“Nakumbuka tulifanya semina na TRA (Mamlaka ya Mapato) na walishindwa kuzijibu hoja za wabunge kwa kuwa zilikuwa za msingi na za kizalendo.

“TTCL ni chombo cha umma kwa gharama za mradi huu wa Sh. bilioni 48, binafsi nashauri serikali ibadilishe mpango wake wa kuajiri watu wa nje kusimamia makusanyo ya kodi hapa nchini.

“'Unapo-surrender' kwa kampuni ambayo ina matatizo makubwa duniani, naiomba serikali hii shughuli ifanywe na TTCL ambacho kina uwezo na ni chombo cha umma.

“Mwaka 2008, tulishauri serikali kuhusu wizi wa mtandao wa simu, serikali ikang’oa mtambo, wakatuambia walinunua kumbe hawakununua, walimweka mwekezaji ambaye kaja na mtambo wake kwa gharama kubwa ya Sh. bilioni 50, wakaingia mkataba wa miaka 15, kitu ambacho si sahihi.

“Masuala ya mtandao wa fedha kama ni mali ya 'vendor' utapigwa tu na tumepigwa na tutaendelea kupigwa. Mimi hoja yangu, tulihoji hata gharama za mtambo wenyewe.

Kwenye semina tumeambiwa mkataba wake ni miaka mitano.“Kuna nchi nyingi wameweka hii 'system' (mfumo), kuna kitu kinaitwa 'new generation' hoja kubwa ni makusanyo. Naomba Waziri wa Fedha alitazame hili ili tupunguze gharama za uendeshaji. Chombo hiki kiendeshwe na mamlaka ya umma ya Tanzania."

Hoja hiyo ya Zungu iliungwa mkono na Mbunge wa Mvomero, Sadiq Murad, ambaye alisema makubaliano ya serikali na kampuni hiyo kutekeleza mradi huo yanakwenda kuongeza gharama za bidhaa husika.

No comments:

Post a Comment

paulmkale