Ibrahim Ajib amerejesha matumaini ya Simba kusonga mbele kwenye michuano ya Mapinduzi Cup baada kupachika kambani bao pekee ambalo limeipa Simba ushindi na pointi tatu muhimu kwenye mchezo wa kundi A uliopigwa usiku kwenye uwanja wa Amaan.
Kikosi cha Simba kilichocheza mchezo wa leo dhidi ya URA kilikuwa kimebadilika kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na kile kilichocheza dhidi ya Jamhuri, timu iliyoanza leo ilikuwa imesheheni wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza ambacho kocha Dylan Kerr amekuwa akikitumia kwenye michezo ya ligi.
Simba walitawala kipindi cha kwanza kwa asilimia nyingi na hiyo ndiyo iliwasaidia kupata goli ambalo lilifungwa na Ajib dakika ya 37 ya kipindi cha kwanza.
Simba imefikisha jumla ya pointi nne na kuongoza Kundi A baada ya kushinda mchezo wa leo. Kwenye mchezo wa kwanza, Simba ilikutana na Jamhuri kutoka kisiwani Pemba na kulazimishwa sare ya kufungana kwa magoli 2-2.
Mchezo wa awali uliochezwa leo majira ya saa 10:15 jioni uliikutanisha JKU dhidi ya Jamhuri ambapo Jamhuri imejikuta ikitepeta mbele ya JKU kwa kukubali kibano cha magoli 3-0.
Kwa maana hiyo, Simba inaongoza kundi kwa pointi nne ikifuatiwa na URA ambayo inapointi tatu sawa na JKU lakini timu hizo zinatofautina magoli ya kufunga na kufungwa wakati Jamhuri tayari imeaga mashindano hayo kutokana na kuwa na pointi moja hadi sasa ikisubiri mechi ya mwisho ya kukamilisha ratiba dhidi ya URA.
Simba yenyewe itacheza mechi yake ya mwisho ya kundi A dhidi ya JKU ambapo inahitaji sare tu ili kusonga mbele ya mashindano lakini ikiwa itapoteza mchezo huo itasubiri matokeo ya mchezo kati ya URA dhidi Jamhuri.
No comments:
Post a Comment
paulmkale