By Sauli Giliard, Mwananchi Digital
Dar
es Salaam. Rais mstaafu Benjamin Mkapa amesema yuko tayari kufanya kazi
yoyote na kutoa ushirikiano wake kwa serikali ya Rais John Magufuli
endapo atahitajika.
Mkapa
aliyeambatana na Waziri Mkuu Mstaafu Joseph Warioba ametoa kauli hiyo
leo punde baada ya kukutana na Rais John Magufuli Ikulu, Dar es Salaam.
“Rais
Mstaafu Mkapa pia amemhakikishia Rais Magufuli kuwa yuko tayari kutoa
ushirikiano wakati wote ama kufanya kazi yoyote endapo atahitajika
kufanya hivyo,” taarifa iliyotolewa na Ikulu leo mchana imeeleza.
Kwa
mujibu wa Ikulu, malengo ya mkuu huyo wa zamani wa nchi kukutana na Rais
Magufuli ni kumpongeza kwa dhamana aliyopewa na Watanzania kuiongoza
nchi, kuunda serikali na kumtakia heri ya Mwaka Mpya.
Taarifa
hiyo imeongeza kuwa, waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba amempongeza
katika juhudi zake katika kusimamia ukusanyaji wa mapato, kubana
matumizi na kuelekeza matumizi kwenye maeneo muhimu ambayo yanawahusu
wananchi yakiwemo afya na maji.
Aidha
taarifa hiyo imeeleza kuwa Jaji Warioba amewataka Watanzania wote
kumuunga mkono Rais Magufuli kwa kazi anazofanya ikiwemo kukomesha
rushwa, ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka na wizi wa mali ya umma.
"Lazima
kila mmoja amuunge mkono Rais, tusije tukamuachia, pale ulipo kama ni
mambo ya rushwa uanzie hapo hapo, kama ni mambo ya matumizi mabaya ya
madaraka anzia hapohapo, tusije tukamuachia Rais pekee yake, yeye awe
kiongozi wetu, lakini Watanzania wote tushughulike na matatizo hayo,"
amesisitiza Jaji Warioba.
No comments:
Post a Comment
paulmkale