Samatta apewa uraia wa DR Congo

Samatta apewa uraia wa DR Congo

GUMZO ni Mtanzania Mbwana Samatta kutwaa Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Afrika kwa wanaocheza soka Afrika. Mitandao mbalimbali na vyombo vya habari jana Ijumaa viliripoti tofauti kwa kumvika uraia wa nchi nyingine Samatta.
Mtandao maarufu wa Wikipedia uliandika Samatta ni raia wa DR Congo inapotokea timu ya TP Mazembe anayochezea straika huyo.
Mtandao wa NBC wa Marekani ukaandika mshambuliaji huyo wa zamani wa Simba ni raia wa Tunisia.
Hali hiyo ilizua sintofahamu kwa watu wengi lakini baadaye Wikipedia walibadili na kuandika Samatta ni raia wa Tanzania.
Samatta hadi anatwaa tuzo hiyo, katika fainali aliwapiku Robert Kidiaba anayecheza naye TP Mazembe raia wa DR Congo. Pia alimzidi raia wa Algeria, Bounedjah Baghdad anayechezea Etoile du Sahel.
Kwa upande mwingine, mastraika wa Yanga, Donald Ngoma na Amissi Tambwe wote walimpongeza Samatta na kusema ameonyesha kweli yeye ni mchezaji bora Afrika.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Tambwe raia wa Burundi, akiwa na Ngoma ambaye ni raia wa Zimbabwe, walimtumia Samatta meseji za kumpongeza kutokana na kutwaa tuzo hiyo.
“Tulimpongeza kwa kutwaa tuzo ya uanasoka bora Afrika, hii inadhihirisha yeye ni bora na sisi tunakubali uwezo wake. Samatta ametutoa kifua mbele watu wa Afrika Mashariki,” alisema Tambwe ambaye nchi yake Burundi inaunda Umoja wa Afrika Mashariki.
“Samatta ana uwezo mkubwa sasa, ameisaidia Mazembe kutwaa ubingwa wa Afrika, kweli huyu ni bora Afrika na tunampongeza kwa kweli.
“Hii ni nafasi ya wachezaji wengine siyo wa Tanzania tu bali wote tunaotoka Afrika Mashariki kujituma na kufanya vizuri zaidi.”
Samatta alitarajiwa kuwasili jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia leo akitokea Lagos, Nigeria kulikofanyika sherehe za utoaji wa tuzo hizo zinazoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

No comments:

Post a Comment

paulmkale